Ikulu ya Marekani imemsimamisha kazi kwa muda bila malipo mmoja wa waendeshaji wa muda mrefu wa teleprompter wa Rais Donald Trump, baada ya kudaiwa kutumia taarifa za ndani kujipatia zaidi ya dola 100,000 kupitia ubashiri wa hotuba za rais kwenye jukwaa la kamari la mtandaoni.
Msemaji wa Ikulu, Karoline Leavitt, amesema hatua hiyo imechukuliwa kufuatia tuhuma zinazomkabili mfanyakazi huyo, huku akibainisha kuwa hatashiriki katika shughuli za rais hadi uchunguzi utakapokamilika.
“Rais anaamini jambo hili ni la kusikitisha sana, na mhusika amewekwa kwenye likizo ya lazima bila malipo,” alisema Leavitt wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, mtuhumiwa huyo ametajwa kuwa ni Gabriel Perez, msaidizi wa kiufundi ambaye amekuwa akiendesha teleprompter ya Trump tangu mwaka 2016.
Inadaiwa Perez alitumia taarifa alizokuwa akizifahamu mapema kuhusu hotuba za Trump kuweka ubashiri kwenye tovuti ya Kalshi, ambayo inaruhusu watumiaji kubashiri ikiwa maneno au mada fulani zitatamkwa katika hotuba.