RAIS DKT. MWINYI" KUIMARISHA MIFUMO YA AFYA NI NJIA BORA YA KUENZI URITHI WA MZEE MKAPA"

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Msarifu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema heshima kubwa inayoweza kutolewa kwa Hayati Rais Benjamin William Mkapa ni kuendelea kuwekeza katika uongozi, kuimarisha mifumo ya afya na kuwawezesha vijana kuwa wasanifu wa mustakabali wa Afrika

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 16 Julai 2026, katika Jukwaa la Nne la Kuuenzi Urithi wa Mkapa pamoja na maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation hafla iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Amesema Hayati Rais Mkapa aliamini kuwa maendeleo endelevu yanajengwa katika misingi ya uongozi imara, taasisi madhubuti na uwekezaji kwa watu, hususan vijana, ili wawe chachu ya mabadiliko katika jamii.

Rais Dkt. Mwinyi amesema imani hiyo ndiyo iliyochochea kuanzishwa kwa Taasisi ya Benjamin William Mkapa miaka 20 iliyopita na imeendelea kuwa msingi wa mafanikio, uimara na uendelevu wa taasisi hiyo.

Ameeleza kuwa, akiwa Mrithi wa Mwanzilishi wa Taasisi hiyo, ana wajibu wa kuhakikisha maono na maadili aliyoyasimamia Hayati Rais Mkapa yanaendelea kulindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, amesema maandalizi ya viongozi wa afya wa Afrika wa siku zijazo yanahitaji kuimarishwa kwa mifumo ya afya, uwekezaji katika rasilimali watu na kuundwa kwa fursa zitakazowawezesha vijana kufikia uwezo wao kikamilifu.

Akizungumzia mchango wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation, Rais Dkt. Mwinyi amesema kwa kipindi cha miaka 20, taasisi hiyo imekuwa mshirika wa kuaminika wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika maendeleo ya rasilimali watu wa sekta ya afya, mageuzi ya mfumo wa afya, uimarishaji wa huduma za afya ya msingi na utekelezaji wa programu za afya ya jamii.

Rais Dkt. Mwinyi ametunukiwa Tuzo Maalumu ya kuthamini na kutambua mchango wake katika maendeleo ya Taasisi ya Benjamin William Mkapa, aliyokabidhiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi.

Naye Rais Dkt. Mwinyi amemkabidhi Mhe. Dkt. Nchimbi Tuzo ya Juu ya Uongozi katika Mageuzi ya Afya, Pinnacle Award for Health Transformation Leadership, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua uongozi na juhudi za Rais Dkt. Samia katika kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya afya, kufanya mageuzi ya mifumo ya afya, kupanua miundombinu na kusukuma mbele ajenda ya kufikia Huduma za Afya kwa Wote nchini Tanzania.

Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Nchimbi, pia amekabidhi Tuzo Maalumu ya kuthamini na kutambua mchango wa Mwanzilishi na Mlezi wa Taasisi hiyo, Hayati Benjamin William Mkapa, iliyopokelewa na Mama Anna Mkapa.

Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru washirika wa maendeleo, taasisi za sekta binafsi, asasi za kiraia, taasisi za elimu na marafiki wa Benjamin William Mkapa Foundation kwa mchango wao katika kuimarisha mifumo ya afya, kuendeleza rasilimali watu na kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.

Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano ili kujenga Afrika yenye watu wenye afya bora, ustawi mkubwa na uwezo wa kustahimili changamoto.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliyemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,Mama Anna Mkapa, viongozi wa Serikali SMZ na SMT, Mabalozi, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Yakub Janabi, Taasisi mbalimbali za Kimataifa, Wadau wa Maendeleo, Wataalamu wa Afya na wageni waalikwa.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii