Marekani imeongeza mashambulizi yake dhidi ya Iran kwa kushambulia madaraja muhimu na kuangusha mnara wa kudhibiti usafiri wa baharini katika bandari ya Chabahar.
Iran nayo imejibu kwa kurusha makombora kuelekea Qatar, Bahrain na Kuwait, huku mapigano yakizidi kuongezeka baada ya kusambaratika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Jeshi la Marekani limesema lilishambulia makumi ya maeneo kusini mwa Iran usiku wa kuamkia leo, yakiwemo madaraja yanayounganisha mji wa Bandar Abbas na maeneo ya ndani ya nchi pamoja na mnara katika bandari ya Chabahar. Iran inasema watu wasiopungua 38 wameuawa na zaidi ya 400 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.
Akizungumza kwa njia ya televisheni, Rais Donald Trump amesema operesheni ya Marekani inaendelea vizuri na matokeo yake yataonekana hivi karibuni.
Kwa upande wake, Iran imerusha makombora kuelekea Qatar, Bahrain na Kuwait, huku Jordan ikisema ilidungua makombora matatu yaliyokuwa yakielekea katika anga yake. Wakati huohuo, meli moja ya mafuta ilishambuliwa katika Mlango wa Hormuz lakini haikupata uharibifu mkubwa wala majeruhi.
Mvutano huo unaendelea kutishia usafirishaji wa mafuta duniani kupitia Mlango wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya biashara ya nishati duniani.