Morocco imesema iliionya Hispania mapema kwamba uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutorejesha haraka wahamiaji wanaowasili kwa njia ya bahari ungeweza kusababisha ongezeko kubwa la watu kuvuka kuelekea eneo la Ceuta.
Afisa mmoja mwandamizi wa Morocco amesema serikali yake ilianza kuwasiliana na Hispania kati ya Julai 22 na 23 baada ya mitandao ya wahamiaji kuanza kusambaza taarifa kuhusu uamuzi huo wa mahakama uliotolewa mwezi Julai tarehe 8 na kwamba uamuzi huo ungeleta changamoto ya wahamiaji kujaribu kuvuka mpaka.
Wiki iliyopita, takriban watu elfu hamsini, wengi wao raia wa Morocco, waliingia Ceuta kwa kutembea au kuogelea kutoka mji wa Fnideq, Idadi hiyo ilizidi uwezo wa mamlaka za Hispania, kabla ya maelfu yao kurejeshwa Morocco.
Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Hispania Elma Saiz amekanusha na kusema kuwa hakukuwa na taarifa yoyote iliyoionya serikali kuhusu ukubwa wa tukio hilo.
Morocco inasema usimamizi wa uhamiaji si jukumu lake pekee, ikisisitiza kuwa itaendelea kupokea wahamiaji wanaorejeshwa kutoka Hispania na kuendeleza ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili katika kudhibiti uhamiaji