Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa makubaliano kuhusu kuufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz yanaweza kutangazwa hivi karibuni. Ameyasema hayo huku Iran na Oman zikikaribia kufikia makubaliano kuhusu njia hiyo.
Akizungumza wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni cha Fox News cha Marekani, Trump ameendelea kusisitiza kuwa nchi yake itaichukulia Iran hatua kali kama mmazungumzo hayatafanikisha njia ya Hormuz kufunguliwa.
Amesema, "Mlango Bahari wa Hormuz utafunguliwa karibuni, vinginevyo watakabiliwa na mashambulizi makali sana, na kwa vyovyote utafunguliwa. Tutaanzisha mashambulizi makubwa sana, makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu Vita vya Pili vya Dunia.''
Mashambulizi ya meli licha ya matumaini ya makubaliano
Kufungwa kwa njia hiyo muhimu kumesababisha kupanda kwa bei ya mafuta kwenye masoko ya kimataifa. Licha ya matumaini kuhusu kupatikana kwa makubaliano, mashambulizi dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu na Mlango Bahari wa Hormuz yameendelea kuripotiwa ambapo waasi wa Kihouthi wa nchini Yemen wamesema wameishambulia kwa makombora meli ya mafuta ya Saudi Arabia nje kidogo mwa Pwani ya Yanbu.