Shirika la kufuatilia usalama wa shughuli za baharini la Uingereza, UKMTO, limesema meli moja ya mizigo imeshambuliwa kwa kombora lisilojulikana upande wa Oman kwenye Mlango wa Bahari wa Hormuz.
UKMTO haikutoa taarifa zaidi kuhusu meli hiyo, ikiwemo bendera ya taifa ililokuwa ikipeperusha au iwapo ilikuwa imebeba mizigo.
Tukio hilo limetokea wakati Marekani na Iran zikitoa kauli zinazokinzana kuhusu iwapo zinafanya mazungumzo kati yao.
Jana Jumatatu, Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema pande hizo mbili zinarejea kwenye mazungumzo kwa lengo la kumaliza vita.
Hata hivyo, Iran imekanusha madai hayo, ikisisitiza kuwa imezungumza na Oman pekee, na kwamba mazungumzo hayo yalihusu hali ya usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.