Mawaziri Ukraine Na Urusi Kukutana Leo Uturuki.

KUFUATIA  shambulio la hospitali ya wajawazito na watoto katika Mji wa Mauripol nchini Ukraine kutoka kwa majeshi ya Urusi, mawaziri wa mambo ya nje wa pande zote mbili leo Alhamisi, Machi 10, 2022 wanatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo ya amani ili kutafuta suluhu ya namna ya kumaliza vita hiyo.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufanyika katika Mji wa Antalya Kusini mwa Uturuki ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba amesema atakutana uso kwa uso na hasimu wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kutoa taswira halisi ya namna ya kumaliza vita hiyo ambayo imeingia katika wiki ya tatu sasa pasipo kupatikana kwa suluhu.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelielezea shambulizi la hospitali hiyo kuwa la kutisha na akisisitiza pande zote mbili kusitisha mapigano hayo kwa faida ya wananchi wasiokuwa na hatia huku Marekani ikiwashutumu Urusi kwa kutumia mbinu za zisizofaa za kivita kuwaathiri raia wa kawaida.

Kwa upande mwingine, Balozi Msaidizi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Dmitry Polyanskiy amesema hospitali iliyopigwa makombora ilikuwa imegeuzwa kama ngome ya kivita na wanajeshi wa Ukraine katika mji huo ambao umezingirwa na majeshi ya Urusi kwa siku kadhaa sasa.

Juhudi za kusitisha mapigano kwa muda ili kuwaokoa wakazi zaidi ya 400,000 wa mji huo, zimekuwa zikigonga mwamba kutokana na majeshi ya Urusi kugoma kusitisha mapigano katika eneo hilo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii