Maandamano dhidi ya shambulizi dhidi ya dereva wa kike Kenya huku 200 wakikamatwa

Polisi nchini Kenya wamewakamata zaidi ya waendeshaji 200 wa boda boda katikati mwa jiji la Nairobi huku msako mkali dhidi ya sekta hiyo ukizidi kufuatia unyanyasaji wa kingono wa dereva wa kike kwenye barabara ya Wangari Maathai.

Inspekta Mkuu wa polisi Hillary Mutyambai alitangaza hayo Jumanne. Idadi hiyo iliongezeka kutoka 32. Zaidi ya pikipiki 12 zimezuiliwa.

Hapo awali, polisi walisema ni watu 16 pekee waliotambuliwa na kuhusishwa na shambulio dhidi ya mwanamke huyo.

Jaji mkuu wa Kenya Martha Koome akilaani kitendo hicho amesema kuna haja ya kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya visa kama hivyo vya unyanyasaji ili wajihisi salama katika nchi yao .

Koome alisema ni jambo la kusikitisha kwa shambulio hilo kufanyika katika mkesha wa siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Amesema mashirika na idara za serikali zinafaa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba visa kama hivyo havitokei .


Leo maandamano yamefanyika jijini Nairobi kulalamikia tukio hilo .Mamia ya watu walijitokeza wakiwa na mabango kutaka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya waendesha boda boda waliomshambulia mwanamke huyo


TH


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii