Mfalme wa zamani wa Uhispania Juan Carlos aamua kuishi UAE

Mfalme wa zamani wa Uhispania Juan Carlos amesema ataishi mjini Abu Dhabi licha ya kukamilika kwa uchunguzi kuhusu shughuli zake za kifedha zilizosababisha kujipeleka mwenyewe uhamishoni katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Juan Carlos amemuandikia barua mtoto wake ambaye ndiye mfalme wa sasa wa Uhispania Felipe VI, kuwa kwa sasa amependelea kwa sababu za kibinafsi zisizomhusu yeyote ila yeye, kuendelea kuishi kwa njia ya kudumu na imara mjini Abu Dhabi. Tangazo la Carlos limekuja siku tano baada ya mwendesha mashitaka wa Uhispania kuchapisha uamuzi wake wa kuufuta uchunguzi wa kesi tatu dhidi yake. Juan Carlos alikwenda mwenyewe uhamishoni katika Umoja wa Falme za Kiarabu mwaka wa 2020 kutokana na uchunguzi huo, ambao ulijumuisha tuhuma za kandarasi haramu zinazohusishwa na mradi wa barabara ya reli ya treni za mwendo kasi nchini Saudi Arabia ambazo zilipewa kundi moja la makampuni ya Uhispania mwaka wa 2011.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii