Serikali kuifumua sheria ya ndoa

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema serikali ipo katika majadiliano na mapitio ya sera ili kubadili sheria ya ndoa ambayo imekua ikileta changamoto katika kusimamia suala zima la ukatili wa watoto.

Waziri Dkt. Gwajima amesema Mkanganyiko wa Sheria ya ndoa unaonekana na wadau wanaohusika wamefikisha malalamiko katika wizara hiyo na wapo katika mpango wa kuhakikisha sheria zote zinakwenda sambamba ili kuleta jamii yenye maridhiano na kupunguza ukatili.

“Malalamiko hayo tumeyapokea na yanaleta mijadala, hii sheria ya ndoa inasema mtoto aolewe na miaka 18, na nyingine miaka 14, hii inakinzana na ni moja ya changamoto katika juhudi hizi, hili ni eneo ambalo lipo mezani na tunalifanyia kazi pamoja na wadau ili kuona kwamba tunafanyaje ili zisigongane. Na baada ya hapo tutapeleka Bungeni ili waone wanapitishaje na sisi ni ‘machinery’ ya kuhakikisha kila wizara inakwenda sawa isiwe wizara hii inakwenda na A, mwingine B+ inakuwa mgongano, tafrani kwenya jamii, kwa hiyo siwezi kusema itakuwaje mbele ya safari ila tunalijadili,” amesema Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali ina mpango kazi wa Taifa wa kupinga ukatili kwa miaka mitano na kila mpango huo unaotekelezwa unafanyiwa tathmini ya yale yaliyofanyika kwa muhula na wakati mwingine masuala yaliyomo huendelea kwa kipindi kinachofuata.

Amesema katika mpango kazi unaeoeleka ukingoni kwa kipindi hiki umeangalia vipengele vyote vinavyoleta ukatili katika familia kama uchumi wa kaya, mila na desturi, elimu ya familia, ukeketaji, mazingira salama, malezi na mahusiano, utekelezaji wa usimamizi wa sheria, utoaji wa huduma kwa waathirika wa ukatili, mazingira salama shuleni, na uratibu na ufuatiliaji.

“Tumefanikiwa maeneo mengi katika hayo niliyoyataja, lakini suala la ukatili na huduma kwa waathirika wa ukatili, ilitakiwa kamati za kijamii ziundwe, na jukumu lake ndio kuangalia wapi pananukia ukatili, taarifa zimeletwa, na madawati ya jinsia yapo yameundwa, baadhi ya hospitali kubwa yana dawati la mkono kwa mkono na kesi zinashinda, tunashirikiana na wadau kwa namba 116 ambayo watu wanatoa taarifa kuhusu ukatili wa mtoto ambayo inasaidia kupunguza hizi kesi, kwa hiyo tumepokea taarifa nyingi sana katika eneo hili na tumeyashughulikia.

Aidha Dkt. Gwajima amesema katika maisha yake na wizara hii ya anayoisimamia suala la ukatili wa wanawake linamsumbua akili na analishughulikia kwa kila hali kuhakikisha linapungua na kuisha kwa haraka.

“Mimi ule ukatili anaopambana nao mwanamke, ukatili wa nguvu, Ukatili wa kiuchumi, mwanamke anaepambana kujiokoa yeye na watoto wake wakiwepoe wanaume, alafu wote hawa wakikua tena wanaanza kumkatili tena mwanamke aliehangaika nao. Mimi naanza kujiuliza huyu mwanamke aliyepitia madhila yote haya, mateso aliyoyapata mwanamke huyu mbona hakuwaacha watoto wake wa kiume? Amesema Dkt. Gwajima.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii