Marekani yakataa pendekezo la Poland kutuma ndege Ukraine

Marekani imelikataa pendekezo la Poland la kutowa ndege za kijeshi za enzi za Kisovieti ili zikabidhiwe kwa Ukraine katika kuisaidia kwenye mapambano yake dhidi ya uvamizi wa Urusi, ikisema haliwezi kutetewa.

Makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon, imelikataa pendekezo la kushangaza la Poland kwamba ingeliipa Marekani ndege zake za kijeshi kwa ajili ya kutumiwa na Ukraine, katika kile kinachotajwa kama ishara isiyo ya kawaida ya kutokubaliana wakati washirika wa muungano wa kijeshi wa NATO wakisaka kuwapa nguvu wanajeshi wa Ukraine bila kujihusisha moja kwa moja na uhasama na Urusi.

Msemaji wa Pentagon, John Kirby, alisema siku ya Jumatano (Machi 9) kwamba tangazo la Poland kwamba inakusudia kuwasilisha ndege zake 28 za kjeshi chama MiG-29 katika kituo cha kijeshi cha Marekani cha Ramstein nchini Ujerumani "linazusha wasiwasi mkubwa kuhusiana na ndege za kijeshi kuondoka Marekani na kwenda kituo cha NATO na kuruka kwenye anga ambalo linawaniwa na Urusi katika mzozo wake na Ukraine."

Hata hivyo, Kirby aliongeza kwamba, hata hivyo, wangeliendelea kushauriana na Poland na washirika wengine wa NATO juu ya suala hilo. Tayar, Urusi ilishatangaza kwamba kulisaidia jeshi la anga la Ukraine kutahisabiwa kama kushiriki vita na kutajibiwa kikamilifu.


.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii