Ndege za Urusi zauwa 17 Ukraine

Mamlaka nchini Ukraine zinasema kuwa ndege za kijeshi za Urusi zimefanya mashambulizi mapya kwenye makaazi ya raia katika sehemu za kati na mashariki mwa nchi hiyo. Maafisa hao wanasema kuwa watu wawili, mmoja wao mtoto wa miaka saba, wameuawa kwenye mji wa Chuhuiv mashariki mwa Kharkiv, mji wa pili kwa ukubwa nchini humo. Katika mji wa Malyn ulio kwenye jimbo la Zhytomyr, magharibi mwa mji mkuu Kyiv, watu watano, wakiwemo watoto wawili, wameuawa na mashambulizi ya anga ya Urusi. Makombora mengine yametuwa kwenye viunga vya Kyiv, huku maji, chakula na umeme ukikatwa, kwa mujibu wa Yaroslav Moskalenko, anayeratibu huduma za kiutu kwenye jimbo la Kyiv. Afisa huyo amesema mashambulizi hayo yamefanya iwe shida kuichukuwa miili ya watu watano waliouawa wakati gari yao ilipoangukiwa na kombora na miili mingine 12 kwenye hospitali ya wagonjwa wa akili, ambako pia wagonjwa 200 wamenasa wakiwa hawana chakula wala dawa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii