MWAKA mmoja! Mwaka mmoja wa Utumishi
uliotukuka, uzalendo, upendo na utu. Mwaka mmoja wa ushujaa kwake na
kwa watanzania. Mwaka mmoja wa historia.
Tutarudi hapa kwenye mwaka mmoja siku nyingine, Tuendelee.
Duniani
kote leo ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake, nami katika bandiko hili
nimechagua kuadhimisha Siku hii na Mwanamke shupavu, jasiri, mvumilivu
na mwenye upendo kwa watanzania kuliko hata ilivyo kwa familia yake.
Ni
wengi wanaweza kuwa Wanawake Majabali katika Taifa letu, lakini huyu
naemzungumzia leo katika Siku hii ya Wanawake ni Mwanamke ambaye
Mwenyezi Mungu amemuinua katikati ya Wanawake wenzie na Wanaume wa Taifa
hili.
Mwanamke ambaye baada ya Taifa kuingia Kwenye jaribio la
kumpoteza Rais wa Nchi (Hayati Dk John Magufuli) macho yetu yakatua
kwake ili aweze kutuvusha kama Rais wetu.
Tanzania haikuwahi kumpoteza Rais akiwa madarakani, lakini Mwaka jana (2021) ilitokea kwa mara ya kwanza.
Katiba ikamtaka Makamu wa Rais achukue Nchi, naye akaapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wafitini
na wenye chuki wakadhani hatoweza, Tazama vichwa vyao viko chini kwa
namna alivyofanya kazi kubwa ya kuijenga Tanzania yetu Kiuchumi,
Kijamii, Kisiasa na Kimataifa.
Happy Women Day, Rais Samia Suluhu Hassan, Heri ya Siku ya Wanawake Shujaa wetu na kiongozi wetu.
Mwenyezi
Mungu alikuinua ukawa Makamu Mwenyekiti katika Bunge lile gumu la
Katiba lakini ukafanikiwa kuwa kipenzi cha kila mjumbe.
Allah
akakuinua tena mwaka 2015 ukawa Makamu wa Rais wa kwanza Mwanamke,
ukafanya kila mtanzania avutiwe na wewe. Kila mtanzania amuite mtoto
wake wa kike Samia.
Wakati tukidhani imetosha, jina lako
linachorwa tena na Mwenyezi Mungu kuwa Rais wa Kwanza Mwanamke wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Bado umeweka rekodi nyingine
kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza Mwanamke wa Chama Cha Mapinduzi CCM
(Taifa), tuseme nini juu yako wewe Mwanamke mwenye upendo na ngozi ya
uongozi?
Nina mengi ya kusema kwenye mwaka mmoja wako wa Urais
Mama lakini wacha niyahifadhi kwa ajili ya kilele chenyewe cha mwaka
mmoja.
Leo nikutakie Siku Njema ya Wanawake huku nikikuomba
utambue kwamba kupitia wewe Wanaume wengi wamebadilisha mitazamo yao
kuhusu watoto wa kike, kupitia wewe Tanzania itazalisha Wanawake wengi
majabali na wenye wivu wa maendeleo.
Kupitia wewe ipo siku
atazaliwa Samia mwingine katika Taifa hili hili lililomzaa Bibi Titi
Mohamed, Amina Salum, Asha Rose Migiro, Maria Nyerere, Fatma Karume na
wengineo wengi.