Mamlaka nchini Australia zimeonya hii leo juu ya ongezeko la mvua zaidi mwishoni mwa juma katika mikoa kadhaa iliyokumbwa na mafuriko mashariki mwa nchi hiyo. Mvua hizo huenda zikatatiza juhudi za kutoa misaada wakati maafisa wa ulinzi wakijaribu kufikia miji iliyoathiriwa zaidi. Mvua zilizonyesha kwa wiki moja katika maeneo kadhaa ya kusini mwa Queensland na kaskazini mwa New South Wales zimesababisha uharibifu mkubwa, kuwaacha maelfu ya watu bila makaazi, kusomba mali, mifugo na kuharibu barabara. Watu 13 wamefariki tangu mvua zilipoanza. Huduma za dharura zimetahadharisha juu ya mvua za radi. Wakati huohuo, baadhi ya raia wameanza kurudi katika makaazi yao siku ya Ijumaa ili kuondoa uchafu na tope baada ya viwango vya maji kupungua huku kukiwa na afueni ya mvua.