Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema tiketi zitakazotumika wakati wa safari za treni ya kisasa ya umeme SGR zitatumia mfumo wa kielektroniki katika hatua zote za ukaguzi wa kuingia, ndani ya treni na wakati wa kushuka.
Utaratibu huo unatajwa ikiwa ni miezi mitano imebaki kabla ya safari za treni za abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kuanza.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Machi 7, 2022 na Mkurugenzi wa Tehama TRC, Injinia Senzige Kisenge wakati akitoa ufafanuzi kwa Kamati ya Bunge ya Bajeti inayotembelea mradi wa ujenzi wa treni ya umeme iendayo kasi (SGR).
“Treni hii na zile za zamani kuna utofauti mkubwa sana, kwanza kuna ukaguzi wa kisasa zaidi eneo la kwanza kwenye kila kituo vipo unapoingia na unapotoka lazima uscan.
“Akiingia ndani ya treni kuna wasimamizi ambao watakua na mashine za kuscan wao hawaruhusiwi kukata tiketi, atakapokuwa anatoka tutamjua kama
tiketi aliyonayo ndiyo halisi au ni vinginevyo, tunaangalia mara mbili wakati wa kuingia na wakati wa kutoka,” amesema.
Injinia Senzige amesema jengo hilo lina lifti za kawaida pamoja na ngazi za lifti ya umeme zinazowawezesha abiria wote kuweza kufika juu bila tatizo.
Awali Mbunge wa Meatu, Leah Komanya alitaka kujua kuhusu namna gani TRC imejipanga kudhibiti tiketi kwa kila behewa pamoja na utaratibu wa mizigo pamoja na miundombinu kwa wenye ulemavu.
Usafiri kwa abiria utakaotumia reli hiyo ambayo ujenzi wake unakamilishwa kwa kiwango cha Standard Gauge (SGR) unatarajiwa kuanza kutolewa ifikapo Septemba 2022 kwa kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro.
Hatua hiyo inafuatia baada ya ujenzi wa mradi huo kufikia asilimia 95.32 ambapo majaribio ya uendeshaji yanatarajiwa kuanza Aprili baada ya behewa za abiria kuwasili.