Makachero wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wameanzisha msako dhidi ya mwanamume mmoja aliyemshambulia kwa kisu mwajiri wake kabla ya kutoweka na kiasi cha pesa kisichojulikana.
Benjamin Munene Ndiang’ui ambaye alikuwa dereva wa Jane Muraguri anayefanya kazi na Mamlaka wa Ustawi wa Majani Chai nchini (KTDA) aliendesha gari lake hadi eneo la siri kwenye barabara kuu ya Thika na kumshambulia bosi wake kwa kisu.
“Ndiang’ui aliendesha gari hadi eneo la siri la ClayWorks kwenye barabara kuu ya Thika ambako alimdunga usoni mara kadhaa akitumia kisu,” taarifa ya DCI inasema.
Baada ya kutekeleza unyama huo, mshukiwa alijitumia pesa kutoka kwa simu ya bosi wake na kukimbia bosi wake akibaki kwenye gari hilo akibubujikwa na damu.
Mhasiriwa, Muraguri, aliokolewa na mlinzi kutoka kwa kampunzi ya usalama ya BM ambaye alimkimbiza hadi Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa matibabu.
“Alimdunga kwa kisu usoni mara kadhaa kisha akatuma pesa kutoka kwa akaunti ya Mpesa ya mwajiri wake. Mshukiwa aliondoka kwa miguu akiacha nyuma kisu alichotumia kutekeleza mashambuliz hayo,” DCI iliongeza.
Mhasiriwa aliachwa na majeraha mabaya kwenye jicho lake la kulia, pua na mdomo huku sasa akiwa amelazwa katika Hospitali hiyo akiwa katika hali mahututi.
Maafisa wa DCI kutoka kituo cha Ruiru wanaongoza msako wa kumkamata mshukiwa.