CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
kupitia mradi wa VaSPHARD kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa
Serikali wamefanya mafunzo kwa Waganga wa tiba asili na kisha kupima
dawa zao ili waweze kubadilisha mtazamo na tabia katika kuzalisha dawa
kutakakopelekea waweze kutengenza dawa salama,safi na zenye viwango vya
juu na kupata usajili.
Mkuu wa Mradi wa
VaSPHARD Dk. Faith Mabiki alisema kuwa mafunzo hayo yanawakutanisha
waganga wa tiba asili na watengenezaji wa dawa zaidi ya 35 kutoka katika
mikoa mbalimbali ya Tanzania ambao wamekuja na dawa zao zaidi ya 100
ambazo baada ya majadiliano na kujengeana uelewa wa zoezi hilo zitapimwa
na kisha kupewa majibu kujua ubora wa dawa hizo na kuwashauri namna
bora za kuzalisha na kufungasha dawa zao kukidhi viwango vya kimataifa.
“Kwa
hiyo sasa hivi tunajadiliana nao baada ya kuwajengea uelewa na
tunaingia nao makubaliano kisha tutakwenda maabara kufanya vipimo viwili
ambavyo vimewekwa na serikali ili waweze kutengeneza dawa kiusalama
zaidi”. alieleza Dk. Mabiki.
Aliongeza “Ili Serikali iweze
kuzitangaza dawa hizo lazima wapelekwe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali
kuangaliwa vipimo kadhaa kama vile sumu kuvu,vipimo vya wadudu
wanaosababisha magonjwa au dawa kuwa chafu, vipimo vya madini tembo na
Kemikali iliyo ndani ya dawa hizo, na kwa bahati nzuri vipimo hivyo
vyote SUA tunaweza kuvifanya ndio maana mkemia mkuu wa Serikali ametupa
kufanya baada ya kupata hela kidogo kutoka kwa Jumuiya ya wanataaluma wa
Sayansi Afrika tunakwenda kufanya kazi hii”.
Alisemaa kama kweli
Taifa linataka kuona Dawa wanazotengeneza zinachangia afya ya Jamii na
maisha ya wataalamu hao wa tiba asili lazima swala la ubora wa dawa hizo
lizingatiwe hapo ndipo wataweza kulifikia soko kubwa la ndani ya
Tanzania na nje kama ambavyo nchi zingine maarufu kwa uzalishaji wa dawa
hizo wamefikia mfano India na China.
Dkt.Mabiki amesema kuwa
zoezi la upimaji wa dawa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali lina gharama kubwa
kama ambavyo waganga hao wamesema lakini SUA kama taasisi ya Elimu na
Utafiti wanavyo vifaa vya kisasa na bora lakini pia wanao wanafunzi
wanaofanya tafiti hizo kwenye shahada mbalimbali za Juu ambao wanatumia
dawa hizo kuzifanyia utafiti na kupata shahada zao lakini pia waganga
wenyewe wenye hizo dawa wanapata kupimiwa dawa zao bure na kupewa
ushauri wa namna ya kufanya na kisha kuweza kupata usajili baada ya
kukidhi vigezo vya Serikali.
“Kwahiyo hapo tunatengeneza
muunganiko mzuri kati ya watafiti, Waganga wa tiba asili na viwanda
maana hawa ukiwangaalia kazi zao ni viwanda tena vya muhimu sana hasa
ukiangalia jinsi sekta hii ya tiba asili inavyokuwa kwa kasi na kuingiza
fedha nyingi duniani na sisi tunataka kama Chuo na Taifa kuona
wataalamu hawa wa tiba asili wanatengeneza pesa nyingi na kuboresha
Maisha yao na kuchangia pato la taifa” alisistiza Dk. Mabiki.
Mkuu
huyo wa mradi wa VaSPHARD alisema mafunzo hayo ni muendelezo na mafunzo
mengine mbalimbali ambayo yamefanyika huku nyuma lakini pia ni kutokana
na tafiti walizozifanya na kubaini kuwa zipo changamoto kwenye
uzalishaji wa dawa hizo lakini watengenezaji hao hawazijui hasa baada ya
kuchukua dawa kadhaa huko nyuma na kuzipima na kugundua kuwa ni chafu
lakini baada ya kuwaeleza na kuwashauri namna nzuri ya utengenezaji wa
dawa hizo wakaenda kutengeneza na kurudisha dawa hizo zikiwa safi.
Kwa
upande wake Mtaalamu wa tiba asili kutoka Njombe, Flavian Nyakeji
alisema amefurahi kupata nafasi hiyo ya kipekee ya kuelimishwa na kujua
namna ya kutengeneza dawa zenye ubora anazizo na madhara kwa wateja na
watumiaji wao kwa ujumla.
“SUA imetusaidia kwa muda mrefu
kuboresha utengenezaji wa dawa zetu wanataka tufikie viwango vya juu, na
sisi hili ndilo tunalolitaka maana sisi tunaotoka Njombe tunauza Njombe
tuu, linini tutauza Dar es salaamu,lini tutauza Mwanza?, Lini tutauza
Kenya? lini tutauza Ulaya na hii ilitokana na kutengenza kwa Viwango vya
chini lakini sasa tunashukuru Mungu amewanyanyua wataalamu wa SUA sasa
wametengenza nyororo ambao kuna watu wamesoma lakini hawajafanya kwa
vitendo na sisi ambao hatujasoma lakini tunafanya kwa vitendo na kupitia
kwao sasa tunaneemeka maan masoko wanayajua” alisema Nyakeji.
Nyakeji
amesema ameleta dawa kumi kwenye zoezi hilo ili aweze kujua nini kipo
kwenye dawa zake hasa kwa kujua ubora wake na yupo tayari kupata ushauri
wa kitaalamu wa namna ya kuboresha dawa hizo ili ziweze kuwa na viwango
badala ya kuzalisha bila viwango hali ambayo itatunyima usajili na
kutofikia soko la nje.
Mtaalamu huyo wa Tiba asili amesema
kupitia mafunzo na uwezeshwaji huo wa kitaalamu tayari kuna mabadiliko
makubwa kati uzalishaji wa tiba asili nchini na anaamini kuwa
kutafanyika mapinduzi makubwa katika soko la tiba asili nchini na
wataweza kuuza bidhaa zao nchi ya nchi kama ambavyo nchi zingine zinauza
Tanzania.