Viongozi wa ECOWAS wafuta ziara yao nchini Burkina Faso

Viongozi wa Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS wamefuta ziara yao nchini Burkina Faso iliyokuwa na lengo la kukutana na kiongozi wa kijeshi Paul-Henri Damiba. Taarifa ya ECOWAS imesema ziara ya viongozi wake akiwemo rais wa Ghana Nana Akufo Addo, imesitishwa na badala yake watawatuma mawaziri katika siku za usoni. Uamuzi huo unafuatia hatua ya Damiba kusimikwa kama rais wa mpito wa taifa hilo kwa kipindi cha miaka mitatu. Kiongozi huyo wa kijeshi jana alimteua mchumi Albert Ouedraogo kuwa waziri mkuu wa mpito. Damiba aliongoza mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Januari na kumuondoa madarakani rais Roch Marc Kabore akidai kuchoshwa na ongezeko la vurugu za wanamgambo wa Kiislamu. Damiba alitia saini hati ya katiba ya mpito ambayo ilitangaza kwamba uchaguzi utafanyika miezi 36 baada ya kuapishwa kwake.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii