Watanzania wapewa siku 55 Poland

Wakati Serikali ikituma maofisa wa ubalozi wa Tanzania kwa nchi za Ujerumani na Sweden kuwafuatilia Watanzania waliokimbia vita nchini Ukraine, Serikali ya Poland imewapa siku 55 wawe wameondoka nchini humo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki iliyotolewa jana inasema Serikali imetuma maofisa kwenda Poland na Hungary kusimamia utaratibu wa kuwawezesha wanafunzi waliokwama kuingia katika nchi hizo kwa urahisi.

Juzi waziri wa wizara hiyo, Balozi Liberata Mulamula alikutana na kamati ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma nchini Ukraine na akawatoa hofu kuhusu hatima ya watoto wao. Mkutano wao ulifanyika jijini hapa.

“Serikali inafanya mazungumzo na Ubalozi wa Urusi uliopo hapa nchini ili kuweka mazingira salama ya kuwawezesha wanafunzi wa Kitanzania waliokwama Ukraine kuondoka kwa kutumia mpaka wa Urusi kutokana na kukosekana kwa njia mbadala. Nawaomba watulizeni watoto wenu kila mnapozungumza nao ili wasitaharuki,” amesema Waziri Mulamula kwenye taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia imesema waziri amewaondoa hofu wazazi wa wanafunzi takriban 160 wanaosoma katika mji wa Sumy uliopo mpakani mwa Ukraine na Russia.

“Wanafunzi wameruhusiwa kusalia chuoni kwa sababu za kiusalama na uongozi wa chuo umeahidi kuwapa mahitaji na huduma muhimu za kibinadamu kikiwamo chakula,” amesema Balozi Mulamula.

Mmoja wa wanafunzi waliokwama nchini Ukraine, Jesca Mlawa alipozungumza na gazeti hili alisema kwa sasa kila mtu anawasiliana na ndugu zake ili atumiwe nauli ya kurudi nchini.

“Kwa sasa kila mtu na mipango yake na wazazi wake. Kuna wengine watakaa siku nyingi. Wengine wanarudi soon (hivi punde), wengine watakaa siku chache na kuondoka kwa sababu tumepewa 55 days to stay in Poland (siku 55 kuishi Poland),” alisema Jesca.

Baadhi ya wanafunzi alisema hawakuona umuhimu wa kuondoka wakijipa matumaini kuwa vita vitakwisha mapema lakini hali inazidi kuwa mbaya.

“Sisi tuliwahi kuondoka Ukraine kuelekea Poland. Global Link walimtuma mtu aliyekuja kutupokea mpakani mwa Poland. Alituchukua pale na kutupeleka tukala na wengine wakaenda kwa ndugu,” alisema Jesca.

Roman Kotliarevskyi (41), raia wa Ukraine anayeishi Bagamoyo mkoani Pwani kwa mwaka mmoja sasa alisema vita hivyo vina chimbuko la muda mrefu lililoanza tangu mwaka 1994.

“Tangu 1994 baada ya Umoja wa Kisovieti kuvunjika tulianza kupigania uhuru wa kujitawala. Kwa miaka yote kulikuwa na machafuko ila yaliibuka rasmi mwaka 2014 Russia ilipotwaa Rasi ya Crimea katika Bahari Nyeusi iliyopo kusini mwa Ukraine kwa nguvu, mwezi mmoja baadaye walilichukua pia eneo la Donbass,” alisema.

Roman, anayemiliki kampuni inayojihusisha na uuzaji wa vifaa vya ujenzi, alisema vita hivyo vimeathiri miundombunu na binadamu hasa wanawake na watoto.

“Nipo nchini Tanzania na familia yangu ya mke na mtoto mmoja, lakini nchini Ukraine ndiko waliko ndugu zangu wote. Ninapoona mapigano yakiendelea moyo unaumia na kujawa hofu kubwa,” alisema Roman.

Vita hivyo, alisema vitaathiri biashara kati ya Afrika na Ukraine ambayo ni msambazaji mkubwa wa mafuta na gesi asilia si Afrika tu, bali duniani kote.

“Russia na Ukraine ndio wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani. Vita vinavyoendelea kule vitasababisha bei ya mafuta ipande,” alisema Roman.

Kuhusu watalii zaidi ya 900 waliokwama visiwani Zanzibar, Roman alisema yupo tayari kusaidia kuwapa malazi baadhi yao.

“Wanaweza kuja tukaishi nao lakini pia wengine tukawapa msaada wa mahitaji muhimu kama vyakula na dawa,” alisema.

Wakati mgogoro huo ukiingia siku ya saba, taarifa zinasema jana Russia ilisema maofisa wake wapo tayari kuendelea na mazungumzo ya amani na Ukraine.

“Wajumbe wetu watakuwa tayari kuendelea na mazungumzo,” msemaji wa Serikali, Dmitry Peskov alisema, akibainisha kuwa mazungumzo hayo yalitarajiwa kuanza jana jioni.

Alisema Vladimir Medinsky ambaye ni msaidizi wa Rais Vladimir Putin, ndiye kiongozi wa ujumbe huo utakaozungumza na maofisa wa Ukraine.

Kwa mara ya kwanza, mazungumzo yalifanyika kwenye mpaka wa Ukraine na Belarus lakini hayakuwa na matokeo mazuri. Mazun gumzo hayo yalifanyika Februari 28, siku tano baada ya vita kuanza.

Licha ya mazungumzo hayo, Russia iliendelea kuishambulia miji mikubwa nchini Ukraine kwa kurusha roketi huko Kharkiv, Chernihiv, Sumy, Mariupol na miji mingine ya kimkakati.

“Katika saa 24 zilizopita, watu 21 waliuawa na 112 kujeruhiwa huko Kharkiv, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine,” Mkuu wa Utawala, Oleh Syniehubov alisema.

Kuhusu mkutano wao wa kwanza, Mshauri Mkuu wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy alisema lengo kuu lilikuwa kujadili uwezekano wa kusitisha vita. Awamu ya pili inaweza kufanyika siku chache zijazo katika mpaka wa Poland na Belarus.

Kabla ya mkutano huo, Rais huyo wa Ukraine alisema nchi yake inataka kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo na kuondolewa kwa wanajeshi wa Rusia ndani ya mipaka yake. Russia imesema inataka yapatikane makubaliano yatakayozinufaisha pande zote.

Mkutano wa kwanza ulifanyika siku moja baada ya Rais Putin kuamuru kikosi cha nyuklia kuwa katika hali ya tahadhari. Akizungumza Februari 27, Putin alisema hatua hiyo inatokana na matamshi ya uchokozi yaliyotolewa na viongozi wa Jumuiya ya Kujihami (Nato) kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii