Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza wameibana Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoani Mwanza (MWAUWASA), wakitaka maelezo ya kina kuhusu sababu za kuendelea kuwepo kwa uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo katika wilaya ya Ilemela.
Akiuliza swali katika kikao cha Baraza la Madiwani la halnashauri ya Ilemela, Diwani wa Kata ya Ibungilo, David Lucas, aliibua hoja hiyo akitaka kufahamu ni lini changamoto hiyo sugu ya mgao wa maji usiofuata ratiba katika halmashauri hiyo itapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Akijibu swali hilo, Mkurugenzi wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Ilemela, Salum Lossindilo, alisema kuwa changamoto kubwa inayochangia hali hiyo ni kukatika na kuyumba kwa umeme katika vyanzo vya uzalishaji wa maji.
Ameongeza kuwa uzalishaji wa maji hauteshelezi, ambapo kwa sasa MWAUWASA inazalisha takribani lita milioni 138 za maji kwa siku, wakati mahitaji halisi ni lita milioni 190 kwa siku.
Aidha, alibainisha kuwa katika chanzo cha uzalishaji cha Capri Point, tangu mwezi Machi hadi sasa, umeme umekatika zaidi ya mara 20, huku katika chanzo cha Butimba umekatika zaidi ya mara 17. Hali hiyo imekuwa sababu kuu ya kuwepo kwa mgao wa maji unaojitokeza mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Katika hatua za kukabiliana na changamoto hiyo, Lossindilo alisema kuwa TANESCO wameahidi kushughulikia changamoto ya umeme ili kuhakikisha huduma ya maji inaimarika.
Pia amebainisha kuwa mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza mradi katika eneo la Capri Point, unaolenga kupanua chanzo cha uzalishaji maji ili kuongeza kiwango cha maji kinachozalishwa na kukidhi mahitaji ya wananchii.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime