Nchi za UN zaunda mkataba wa kupambana na platiki

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimekubaliana kuunda mkataba wa kisheria utakaoshughulikia uchafuzi wa mazingira kutokana na taka za plastiki baharini, mitoni na ardhini. Baraza la mazingira la Umoja wa Mataifa limepiga kura kwa kauli moja kupitisha azimio hilo katika mkutano uliofanyika Nairobi nchini Kenya. Rais wa baraza hilo na waziri wa mazingira wa Norway Espen Barth Eide amesema taka za plastiki zimegeuka kuwa janga na azimio hilo linaandika historia mpya. Mkataba huo utaangalia mnyororo mzima wa plastiki kuanzia uzalishwaji hadi namna zinavyoharibiwa. Kwa mujibu wa tathmini za kimazingira za hivi karibuni, viwanda vya plastiki duniani vinakadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 522 na tani za ujazo zipatazo milioni 11 hutupwa baharini ila mwaka. Baada ya wiki nzima ya mdahalo, wajumbe walitoa mapendekezo, moja kutoka Peru na Rwanda na mengine kutoka India na Japan ya kuweka mkakati wa mpango wa kimataifa wa kuzuia na kupunguza uchafuzi wa mazingira kutokana na plastiki.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii