Kilio cha Watanzania waliokwama Ukraine

Wakati majeshi ya Russia yakiendelea kushambulia miji nchini Ukraine, baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini humo wameeleza machungu ya vita hivyo wasijue hatima yao.

Tayari Serikali ya Tanzania imeshatoa maelekezo kwa Watanzania wanaoishi nchini Ukraine ikiwataka kukimbilia kwenye nchi za Poland, Romania, Slovakia na Hungary.

Hata hivyo, akizungumza jana kwa mtandao wa WhatsApp, kiongozi wa wanafunzi katika Chuo Kikuu Sumy State, Dk Lahsen Mohammed Kheir, alisema kuondoka nchini humo kwa sasa ni kuhatarisha zaidi maisha.

“Huku kinachoendelea kila siku ni mabomu tu. Kuamua kuondoka kwenda sehemu nyingine ni kujihatarishia maisha kwa sababu miji yote imezungukwa na majeshi,” alisema.

Alisema kila mabomu yanaporushwa, huwa wanakimbilia kwenye mahandaki yaliyo karibu na vyuo ili kujificha.

Hata hivyo, alisema baadhi ya wanafunzi wa Tanzania waliowahi kuondoka kabla ya uvamizi walifika mpaka wa Poland na kufanikiwa kuvuka.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii