Kiongozi mkuu wa upinzani huko Israel ameikosoa serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa kuielekeza nchi hiyo kwenye "janga la kiusalama." kutokana na uhaba wa wanajeshi.
Yair Lapid ametoa kauli hiyo katika taarifa iliyopeperushwa kwenye televisheni, akiishutumu serikali ya Netanyahu kwa kulitumia kupita kiasi jeshi na baadaye kulitelekeza kwenye uwanja wa vita.
Mwanasiasa huyo amelisifu jeshi la Israel lakini akasema linalazimishwa kupigana vita mbalimbali bila rasilimali za kutosha wala mkakati mahsusi. Kauli ya Lapid imetolewa baada ya mkuu wa majeshi wa Israel Eyal Zamir kuelezea siku ya Jumatano wasiwasi kama huo kwa baraza la usalama la Israel.