MAMLAKA ya Uteuzi imeridhia maombi ya muda wa ziada kwa Tume ya
Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 2025 hivyo imeiongezea tena muda wa siku ishirini na moja (21) na
kuitaka ikamilishe kazi kabla au ifikapo Aprili 24, 2026.
Mamlaka hiyo imeeleza sababu za kuongeza muda huo kwa Tume ni
pamoja na kuiwezesha Tume kukamilisha uchambuzi wa ushahidi, taarifa na maoni
yaliyopokelewa, kutoa fursa kwa wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi kufanyia
kazi baadhi ya vielelezo vipya vilivyowasilishwa.
Sababu nyingine ni kuiwezesha Tume kukamilisha maandalizi ya
Ripoti itakayowasilishwa kwa Rais na kutoa fursa kwa Tume kuandaa tafsiri ya
Ripoti hiyo.
Tume hiyo ilianza kutekeleza majukumu yake Novemba 20, 2025 na
kutarajiwa kukamilisha kazi yake ndani ya kipindi cha siku 90. Hata hivyo,
kutokana na sababu mbalimbali, Tume iliongezewa muda wa kukamilisha kazi na
kutakiwa kuwasilisha Ripoti kwa Rais kabla au ifikapo April 3, 2026.
Hivyo, kufuatia nyongeza ya muda, wananchi waliendelea kujitokeza
kwa wingi tofauti na matarajio ya Tume. Hivyo, Tume iliendelea kupokea
ushahidi, taarifa na maoni zaidi. Kwa sababu hiyo, Tume haikuweza kukamilisha
kazi yake ndani ya muda wa nyongeza uliotolewa na hivyo kulazimika kuomba muda
wa ziada ili kukamilisha kazi yake.
Tume inaendelea kuwashukuru wananchi na wadau wote waliotoa ushirikiano kwa Tume wakati wa kufanya uchunguzi, ikiwemo wale waliofika mbele ya Tume kutoa ushahidi, taarifa na maoni, waliopiga simu na kutuma ujumbe, waliotuma ushahidi, taarifa na maoni kwa maandishi na waliowasiliana na Tume kwa njia za mitandao ya kijamii.