Trump Afunguliwa Kesi Mpya na Democrats Kuhusu Kura za Posta

Chama cha Democrats nchini Marekani kimefungua kesi mahakamani kupinga agizo jipya la Rais Donald Trump linalolenga kudhibiti upigaji kura kwa njia ya posta, wakidai hatua hiyo ni kinyume cha Katiba ya nchi hiyo.

Kesi hiyo imewasilishwa na viongozi wakuu wa chama hicho akiwemo Kiongozi wa Wachache katika Seneti Chuck Schumer na Kiongozi wa Wachache katika Baraza la Wawakilishi Hakeem Jeffries, pamoja na Democratic National Committee na taasisi nyingine za chama hicho.

Democrats wanadai kuwa Katiba ya Marekani inatoa mamlaka ya kusimamia uchaguzi kwa majimbo na Bunge (Congress), si Rais. Wamesisitiza kuwa hatua ya Trump ni jaribio la kuingilia mfumo wa uchaguzi kwa maslahi ya kisiasa.

“Tutakutana naye mahakamani na tutashinda tena,” alisema Schumer katika taarifa yake.

Hii ni mara ya pili kwa Trump kukumbana na changamoto ya kisheria kuhusu maamuzi yake ya uchaguzi, baada ya agizo lake la awali kuzuiwa na mahakama mwaka uliopita.

Upigaji kura kwa njia ya posta umekuwepo kwa zaidi ya karne moja nchini Marekani, lakini ulianza kuwa mjadala mkubwa kisiasa tangu uchaguzi wa mwaka 2020.

Wakati huo, Trump alitoa madai ya udanganyifu mkubwa katika kura hizo, madai ambayo yamekataliwa na uchunguzi mbalimbali, ikiwemo uliofanywa na viongozi wa chama chake mwenyewe.

Cha kushangaza, licha ya kuipinga mara kwa mara, Trump mwenyewe amewahi kupiga kura kwa njia ya posta katika chaguzi mbalimbali.

Kesi hii inaongeza mvutano wa kisiasa kuelekea uchaguzi ujao wa bunge, ambao utaamua iwapo chama cha Trump kitaendelea kudhibiti Congress au la.

Wachambuzi wa siasa wanaamini kuwa uamuzi wa mahakama unaweza kuwa na athari kubwa katika mfumo mzima wa uchaguzi wa Marekani, hasa kuhusu matumizi ya kura za posta.

10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii