Mwanafunzi wa Kenya alivyoshuhudia ubaguzi na mateso kwenye mpaka wa Ukraine na Poland

Fatma Abou ni mwanafunzi anayesomea udakitari nchini Ukraine. Huu ulikuwa mwaka wake wa sita na wa mwisho kabla kumaliza masomo na kuhitimu kama dakitari.

Lakini mashambulizi nchini humo yalisababisha yeye na wanafunzi wengine wengi raia wa Kenya kutorokea Poland.Alisema, masaibu yao siku ya pili baada ya vita kuzukua baina ya wanajeshi wa Ukraine na Urusi. Walitoroka kuelekea Poland ambapo walikumbana na changamoto nyingi.

Alielezea kilichotokea siku ya kwanza ya mashambulio ambapo alisema aliamshwa na simu ya mama yake ambaye alimuuliza iwapo alikuwa salama na kumfahamisha kuwa mji mkuu Kiev umeshambuliwa. Hata hivyo alimfahamisha mama yake kuwa alikuwa umbali was aa mbili kutoka Kyiv.

Alipoamka siku ile kulikuwa na milio ya ving'ora vya tahadhari ya mashambulio ambavyo vilisikika kila mara, hali ambayo anasema ilitisha na baadaye katika kundi la wanafunzi la WhatsApp walifahamishwa kuwa ni wakat iwa kutoroka kufuatia mapigano.

''Baada ya hapo tuliondoka kuelekea boda na kusema kweli njiani kote hatukushuhudia ubaguzi wowote ndani ya Ukraine, ila njiani kulikuwa na vituo vingi vya ukaguzi wa jeshi…ndani ya Ukraine hakukua na ubaguzi, ubaguzi ulikuwa kwenye boda'', anasema.

Yeye na wakenya wenzake walilazimika kutembea kilomita thelathini kufika mpaka wa Poland. Na walipowasili wanasema walikumbana na ubaguzi wa rangi.

''Maafisa upande wa mpaka wa Ukraine walitoa nafasi kwa wanawake na watoto wa Ukraine kuvuka mpaka kwanza huku wanafunzi kutoka nchi za Afrika,waarabu na wahindi wakiwekwa kando''.

Fatma Abou anaeleza ilikuwa hali ya mshike mshike kusukumana kuvuka mpaka huo.

' 'Kupita kwa boda laini ilikuwa ndefu sana…sasa unajua kila mtu alikuwa kwa laini kama ulikuwa mwanamke hata mwanaume alikuwa anaweza kukugusa, kuna mtu alinivuta nywele sijui hata nani alinivuta wallah!!'', anasema Bi fatma huku akicheka, na kuongeza kuwa: ''Baadaye tulitenganishwa White people and black people (watu weupe na watu wetu weusi)''…Ni watu wao, walikuwa wanaokoa watu wao. Kusema kweli sio Waafrika tu kulikwa na Waarabu, Walatino, watu ni wengi sana kulikuwa pia na Wahindi pia'', anaeleza..

Akijibu ni vipi aliweza kujua kuwa wanabaguliwa Bi Fatma alisema: ''Unatandikwa walikuwa katili kusema kweli, unapotaka kupita wanakushikia bunduki, ni lazima usubiri, usiku katika baridi, hata nilizimia…'' ''Kusema kweli wanafunzi wa kigeni walichukuliwa kama takataka kusema kweli … Na ukiingia kwenye kambi unalazimika kusubiri katika baridi, ili upigiwe muhuri''

Bi Fatma ambaye kwa sasa amefanikiwa kuvuka na kuingia Poland anasema wenzake Wakenya hasa wanaume hajawaona tena. Wanaume waliwekwa kando katika upande wa Ukraine wasijue ikiwa wataingia Poland au la.


Kwa sasa Fatma na wanafunzi wenzake wasichana wamepewa malazi, dawa na chakula na maafisa wa huduma ya kwanza wa Poland.

Hawajui hatua itakayofuata kwasababu hakuna wawakilishi wa serikali za nchi zao upande wa Poland katika kambi hizo za wakimbizi.

Fatma anasema ikiwa Kenya haitawasaidia kurudi nyumbani Nairobi, watalazimika kutegemea familia zao kuchanga fedha ili wapate nauli ya ndege kusafiri hadi Kenya.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii