Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Amina, amewahimiza watengeneza maudhui mtandaoni kutumia ubunifu wao kuleta mabadiliko chanya katika jamii, akisisitiza kuwa kazi hiyo si chanzo cha mapato pekee bali pia ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo Aprili mosi, 2026 katika ukumbi wa Gold Crest mkoani Mwanza, alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Mhe. Amina alisema mafunzo hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo washiriki, hususan katika kuboresha kazi zao na kutumia teknolojia kwa ufanisi zaidi.
Alieleza kuwa dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, hivyo ni muhimu kwa vijana kutumia fursa hiyo kujifunza na kujiongezea ujuzi ili kuendana na mabadiliko hayo.
“Utengenezaji wa maudhui una nafasi kubwa katika kuhamasisha jamii na kuleta mageuzi chanya. Ni wajibu wenu kutumia vipaji mlivyonavyo kuimarisha umoja, uzalendo na mshikamano wa kitaifa,” alisema.
Ambapo alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwaunga mkono vijana, hasa wazawa wa Mkoa wa Mwanza, kwa kuwapatia fursa mbalimbali zitakazowawezesha kusonga mbele katika kazi zao na kuchangia maendeleo ya nchi.
Aidha aliwataka watengeneza maudhui kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayoweza kuharibu taswira ya jamii na taifa, akisisitiza umuhimu wa maadili na uwajibikaji katika kazi zao.
Hata hivyo mafunzo hayo yamewakutanisha watengeneza maudhui mbalimbali mkoani Mwanza, yakilenga kuwajengea uwezo wa ubunifu, matumizi sahihi ya teknolojia na namna ya kutumia majukwaa ya kidijitali kuleta maendeleo endelevu.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime