"HOUSE GIRL" AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA KUJARIBU KUUA KICHANGA

​Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, leo Machi 09, 2026, limemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Faima Yasin Twaibu (19), mkazi wa Bulyehele, kwa tuhuma za kujaribu kumuua mtoto mchanga.

​Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Christian Mwalimu, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Evance Kaiza akisaidiana na Clara Muhando, ulidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 25, 2025.

​Inadaiwa kuwa katika mtaa wa Bulyehele, kata na wilaya ya Ilemela, mshtakiwa alijifungua mtoto mchanga na kisha kumtupa juu ya paa la nyumba kwa lengo la kutoa uhai wake.

​Mshtakiwa katika shauri hilo namba 5112/2026, anakabiliwa na shtaka moja la jaribio la kuua, kinyume na Kifungu cha 211(b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

​Akijibu swali la Mheshimiwa Hakimu aliyetaka kujua sababu ya kumtupa mtoto huyo juu ya paa la bati, mshtakiwa alidai kuwa alifikia uamuzi huo kwa hofu ya mwajiri wake (ambaye hakumtaja jina) asigundue kuwa alikuwa mjamzito na amejifungua.

"Sikutaka Boss wangu ajue kama nilikuwa mjamzito na nimejifungua mtoto" alisema Faima 

​Mhe. Mwalimu alieleza kuwa kosa hilo lina dhamana, ambapo mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya Taifa (NIDA) na barua za utambulisho kutoka Serikali za Mitaa. Aidha, kila mdhamini alitakiwa kusaini hati ya dhamana ya Shilingi Milioni Tatu (Tsh 3,000,000).

​Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana na hivyo kupelekwa rumande.

​Kuhusu hali ya mtoto huyo, ambaye kwa sasa ana umri wa miezi miwili na wiki mbili, yupo salama chini ya uangalizi wa Maafisa Ustawi wa Jamii.

Hata hivyo shauri hilo limepangwa kutajwa tena Machi 23, 2026, kwa ajili ya kusomewa hoja za awali na kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii