Idadi ya watu waliofariki katika mafuriko yafikia 42

Polisi nchini Kenya inasema watu 42 ndio wamethibitishwa kufariki hadi sasa kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Kulingana na mamlaka, kati ya 42 hao, 26 waliripotiwa kufariki katika jijiji kuu Nairobi, ambapo makazi na majengo ya kibiashara yalifurika maji huku magari yakisombwa.

Barabara nyingi za jiji la Nairobi, ziligeuka kuwa mito, shughuli za usafiri zikikwama siku ya Ijumaa haswa katika barabara kuu ya Nairobi – Mombasa.

Maafisa wa uokoaji, hadi kufikia wikendi iliopita walikuwa wakiendelea kujaribu kutafuta miili inayodhaniwa kuwa huenda imekwama kwenye matope haswa katika maeneo yenye shuguli nyingi kama eneo la grogan ambako kuna karakana kubwa ya magari.

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, Waziri wa utumishi wa umma Geoffrey Ruku alithibitisha serikali kutuma timu za kukabiliana na majanga katika maeneo yalioathirika zaidi.

Kulingana na Waziri Ruku, serikali pia itagharamia ada ya matibabu kwa watu waliojeruhiwa, wakati huu wizara ya afya ikionya kuhusu uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko, ikiwataka raia kuendelea kuchukua tahadhari hasa wakati huu ambapo mamlaka ya hali ya hewa imeonya kuhusu mvua kunyesha zaidi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii