Watu 3 wa Familia Moja Wafariki kwa Ajali ya Moto Katavi

Watu watatu wa familia moja wamepoteza maisha huku wengine watatu wakijeruhiwa kufuatia ajali ya moto iliyotokea katika Kijiji cha Ilunde, Kata ya Ilunde, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi Region.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Machi 5, 2026 katika Kitongoji cha Miembeni baada ya nyumba moja kuteketea kwa moto. Waliofariki dunia ni Winfrida Sheka (32), Peter Lumilija (9) na Thabiza Lumilija (5). Majeruhi katika tukio hilo ni Paschal Lumilija (37), Ratifa Lumilija (7) na Elisha Lumilija (1), wote wakazi wa kitongoji hicho.

Taarifa zinaeleza kuwa chanzo cha moto huo ni mafuta ya petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa ndani ya chumba cha kupikia kushika moto ingawa inadaiwa kuwa Paschal Lumilija alikuwa akijihusisha na biashara ya kuuza mafuta ya petroli kwa njia ya kienyeji.

Miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi katika Kituo cha Afya Ilunde, huku majeruhi wakiendelea kupatiwa matibabu katika kituo hicho na hali zao zimeripotiwa kuendelea vizuri.

Jeshi la Polisi mkoani Katavi limetoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kwa kuepuka kuhifadhi vitu vinavyoweza kulipuka kama petroli ndani ya nyumba wanazoishi.

Aidha, polisi wamesisitiza kuwa ni kosa kisheria kuhifadhi mafuta ya petroli majumbani badala ya kuyahifadhi katika vituo rasmi vya kuuzia mafuta.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii