Shirika la ndege la taifa, Air Tanzania, limetangaza mpango maalum wa kuwarejesha nyumbani Watanzania waliokwama nje ya nchi kufuatia kusitishwa kwa safari nyingi za ndege kutokana na mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hatua hiyo imekuja baada ya mashambulizi yaliyodaiwa kufanywa na Marekani kwa kushirikiana na Israel dhidi ya Iran, yaliyosababisha kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, Jumamosi iliyopita na kuongeza hali ya taharuki katika eneo hilo.
Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa Machi 6, Air Tanzania imesema ndege maalum itasafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dubai na kurejea tena Dar es Salaam siku ya Jumapili.
Shirika hilo limeeleza kuwa safari hiyo si ya kibiashara, bali ni ya dharura, na kipaumbele kitapewa abiria waliokuwa tayari wamekata tiketi kabla ya safari za ndege kusitishwa.
Aidha wakati huo huo, mashirika mengi ya ndege ya kimataifa yamesitisha safari kuelekea Mashariki ya Kati kufuatia hatua ya Iran kuanza kulipiza kisasi kwa kushambulia kambi za kijeshi za Marekani zilizopo katika baadhi ya nchi za Kiarabu.
Hata hivyo kutokana na hali hiyo, safari za ndege zinazoingia na kutoka katika viwanja vya ndege vya Tel Aviv, Dubai na Doha pamoja na vituo vingine vikubwa vya kimataifa katika eneo hilo zimesitishwa kwa muda.