Serikali ya Gabon imetangaza kufungia matumizi ya mitandao ya kijamii nchini humo, ikieleza kuwa maudhui yanayosambazwa kupitia majukwaa hayo yanachochea vurugu, chuki, udhalilishaji pamoja na magawanyiko katika jamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, baadhi ya taarifa zinazosambazwa mtandaoni ni za uongo na zinahatarisha usalama wa taifa, hali iliyolazimu mamlaka kuchukua hatua za muda kudhibiti hali hiyo.
Hatua hiyo imekuja wakati kukiwa na wasiwasi wa kuongezeka kwa taarifa potofu na uchochezi wa kisiasa unaoweza kuathiri utulivu wa nchi.
Serikali imeeleza kuwa uamuzi huo unalenga kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.
Aidha wachambuzi wa masuala ya haki za binadamu wamekuwa wakieleza kuwa kufungiwa kwa mitandao ya kijamii kunaweza kuathiri uhuru wa kujieleza na haki ya wananchi kupata taarifa.
Hata hivyo Serikali ya Gabon imesisitiza kuwa itafanya tathmini ya hali hiyo na kutoa mwelekeo zaidi kulingana na mwenendo wa usalama nchini humo.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime