BAKWATA Yatangaza Uwezekano wa Ramadhan Kuanza Feb 19 au 20

Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) limetangaza kuwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan unatarajiwa kuanza Februari 19 au Februari 20, 2026, kutegemeana na kuandama kwa mwezi.

Akizungumza na waumini, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA Makao Makuu, Sheikh Hamisi Mataka, amesema Februari 18 itakuwa ni mwezi 29 wa Shaaban, hivyo iwapo mwezi utaandama siku hiyo, Ramadhan itaanza Februari 19.

“Ikiwa mwezi utaandama tarehe 18, basi tarehe 19 tutaingia katika mwezi mtukufu wa Ramadhan. Usipoandama, tutakamilisha siku 30 za Shaaban na Ramadhan itaanza siku inayofuata, InshaAllah,” amesema Sheikh Mataka.

Amesisitiza kuwa Waislamu wanapaswa kusubiri taarifa rasmi kutoka BAKWATA, akibainisha kuwa baraza hilo lina kamati maalum ya ufuatiliaji wa mwandamo wa mwezi kwa kushirikiana na nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Zanzibar na Kenya.

Ameongeza kuwa baada ya kuthibitishwa kwa taarifa ya kuandama kwa mwezi, Mufti wa Tanzania atatoa idhini na tangazo rasmi kwa Waislamu kote nchini kuhusu kuanza kwa mfungo wa Ramadhan.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii