Mamlaka nchini Gabon imetangaza Jumanne kusitishwa kwa majukwaa ya mitandao ya kijamii bila hata hivyo kuyataja, ikisema kuwa maudhui yanayochapishwa mtandaoni yanaweza kusababisha migogoro na mgawanyiko katika jamii.
Hatua hiyo ilitangazwa kwenye televisheni ya taifa na msemaji wa Mamlaka Kuu ya Mawasiliano nchini humo Jean-Claude Mendome aliyesisitiza kuwa "maudhui yasiyofaa, ya kashfa, ya chuki, na ya matusi" yalikuwa yakidhoofisha "utu, maadili ya umma, heshima ya raia, mshikamano wa kijamii, utulivu wa taasisi za Jamhuri na usalama wa taifa la Gabon."
Mamlaka hiyo imeongeza kuwa "kuenea kwa taarifa za uongo", "unyanyasaji mtandaoni" na "ufichuzi wa data binafsi bila idhini" ni miongoni mwa sababu za uamuzi huo. Hata hivyo mamlaka hiyo imesema kuwa "uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kutoa maoni na ukosoaji," unabaki kuwa "haki ya msingi inayolindwa na katiba ya Gabon".
Takriban mwaka mmoja tangu kuchaguliwa kwake, Rais wa Gabon Brice Oligui Nguema amekabiliwa na matatizo ya kijamii kufuatia migomo ya walimu huku watumishi wengine wa umma hasa katika sekta ya afya wakitishia pia kuanzisha mgomo.