Serikali Yaidhinisha Marekebisho ya Katiba ya Simba

Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imeidhinisha rasmi marekebisho ya Katiba ya Simba Sports Club baada ya kukamilika kwa mchakato wa kisheria uliokuwa chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Michezo.

Ikumbukwe kuwa Februari 16, 2026, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alimuagiza Msajili wa Vyama vya Michezo kuhakikisha mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Simba unapatiwa majibu kabla ya mwezi kumalizika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 18, 2026, Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Abel Ngilangwa, amesema marekebisho hayo yamefanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zote zinazosimamia vyama vya michezo nchini.

“Napenda kuufahamisha umma kuwa mchakato wa uchambuzi, tathmini na uidhinishaji wa marekebisho ya Katiba ya Klabu ya Simba umekamilika kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Sura ya 49 na kanuni zake,” amesema Ngilangwa.

Ameongeza kuwa Katiba hiyo iliyorekebishwa iliwasilishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 11 ya Kanuni za Msajili wa Vyama vya Michezo T.S Na. 441 ya mwaka 1999 kwa ajili ya kupitiwa na kuidhinishwa.

Aidha, ameeleza kuwa Msajili alitekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Kanuni ya 11(3)(a), inayomtaka kuhakikisha marekebisho yoyote ya katiba hayaathiri usalama, hayavurugi amani miongoni mwa wanachama au jamii kwa ujumla, wala kuathiri maendeleo ya chama.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii