Kesi ya kupinga uteuzi wa Tume iliyoundwa kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata, imeendelea kusikilizwa leo Alhamisi Februari 26, 2026 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Awamu Mbagwa.
Ambapo shauri hilo limefunguliwa na Watanzania watatu—Rosemary Mwakitwange, Deogratias Mahinyila na Edward Heche—wanaodai kuwa uteuzi wa Tume inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman una dosari za kisheria.
Wanadai kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, misingi ya haki ya asili, matumizi mabaya ya mamlaka na nia ovu katika kuundwa kwake.
Waombaji wamehoji uhalali wa kile wanachokiita “Tume huru ya uchunguzi,” wakidai haijatambuliwa na Sheria ya Tume za Uchunguzi.
Pia wamedai uteuzi huo haukutangazwa kwenye Gazeti la Serikali wala kubainisha wazi madhumuni ya tume kama inavyotakiwa kisheria.
Aidha, wameibua hoja ya mgongano wa maslahi wakisema wengi wa wajumbe ni wastaafu waliowahi kuteuliwa na Rais, jambo linaloweza kuathiri uhuru wao katika kuchunguza masuala yanayohusu mamlaka ya uteuzi hivyo Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi wake Machi 6, 2026.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime