Ndege mbili za kijeshi za Marekani, F-15E Strike Eagle na A-10 Thunderbolt II, zimeripotiwa kuangushwa na mashambulizi ya Iran, huku juhudi za uokoaji zikiendelea kwa baadhi ya wahudumu wa ndege hizo.
Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, mmoja wa wahudumu wa ndege ya F-15E ameokolewa, huku msako ukiendelea kumtafuta mwingine. Katika tukio tofauti, ndege ya A-10 ilishambuliwa lakini iliweza kutua salama nchini Kuwait na rubani wake kuokolewa.
Ndege ya F-15E ni moja ya ndege zenye nguvu kubwa katika Jeshi la Anga la Marekani. Ina uwezo wa kufanya mashambulizi ya anga kwa anga na ardhini katika hali yoyote ya hewa.
Ina kasi inayofikia maili 1,875 kwa saa na inaweza kupaa hadi futi 60,000 angani. Pia hubeba makombora mbalimbali pamoja na bunduki ya milimita 20 yenye risasi 500.
Ndege hii ina wahudumu wawili rubani na mtaalamu wa mifumo ya silaha na ina teknolojia ya kisasa inayomwezesha rubani kuona taarifa muhimu bila kuangalia chini kwenye cockpit.

Kwa upande wa A-10, hii ni ndege maalum kwa kusaidia vikosi vya ardhini, hasa kwa kushambulia magari ya kivita kama mizinga.
Ingawa si ya kasi kubwa (hufikia karibu maili 420 kwa saa), A-10 inajulikana kwa uimara wake mkubwa. Imetengenezwa kustahimili mashambulizi makali na kuendelea kufanya kazi.
Aidha kinga ya chuma (titanium armor) inayomlinda rubani na mifumo muhimu, na inaweza kuhimili mashambulizi ya risasi nzito. Pia ina bunduki kubwa ya Gatling inayoweza kurusha hadi risasi 3,900 kwa dakika.
Hata hivyo tukio hili linatokea wakati mvutano mkali ukiendelea kati ya Marekani na Iran, huku operesheni za kijeshi zikiendelea katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.
10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime