Wanaume waonywa saratani ya matiti

Asilimia moja ya wanaume hupata saratani ya matiti kwa mwaka, hivyo wametakiwa kuwahi hospitali pindi wanapotambua mabadiliko yoyote katika matiti yao, ikiwemo uvimbe, maumivu au kutokwa na majimaji, ili kufanyiwa uchunguzi wa mapema wa afya.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza Zanzibar (NCDs), Dk. Omar Mohammed Suleiman, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa mapema wa magonjwa ya saratani kwa makundi yote ya jamii, kama sehemu ya jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

Dk. Omar amesema kuwa licha ya imani iliyojengeka katika jamii kwamba saratani ya matiti huwapata wanawake pekee, wanaume nao wapo katika hatari ya kuugua, ingawa kwa kiwango kidogo zaidi ikilinganishwa na wanawake.

“Takribani asilimia moja ya wagonjwa wa saratani ya matiti ni wanaume, lakini changamoto kubwa ni kwamba wengi wao hufika hospitalini wakiwa tayari wamechelewa kutokana na kukosa uelewa na dhana potofu kuwa ugonjwa huo hauwahusu,” amesema Dk. Omar.

Amefafanua kuwa dalili za saratani ya matiti kwa wanaume ni pamoja na uvimbe kwenye titi au kwapa, maumivu yasiyo ya kawaida, mabadiliko ya umbo la titi, ngozi kukakamaa, pamoja na kutokwa na damu au majimaji kwenye chuchu.

Amesisitiza kuwa uchunguzi wa mapema una mchango mkubwa katika kuongeza uwezekano wa kupona na kupunguza gharama za matibabu, ikilinganishwa na wagonjwa wanaogundulika wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa.

Aidha, amewahimiza wanaume kuacha aibu na hofu wanapokutana na mabadiliko yasiyo ya kawaida katika miili yao, na badala yake kuwahi vituo vya afya kwa ushauri na uchunguzi wa kitaalamu, akisisitiza kuwa afya ni msingi wa maisha bora.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii