Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, amewataka mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya nchini kutenga muda wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi, hususan migogoro ya ardhi inayosababisha usumbufu kwa jamii.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo wakati wa hotuba yake ya kuahirisha shughuli za Bunge la 13, Mkutano wa Pili, ulioanza Januari 27 mwaka huu.
Amesema viongozi wanapaswa kushuka chini na kusikiliza wananchi wao ili migogoro isikue na kuathiri amani pamoja na maendeleo ya Taifa.
Katika hatua nyingine, Dk. Nchemba amesema serikali inaendelea kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora katika ngazi zote kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wa Kitanzania kupata ujuzi unaowawezesha kushindana kitaifa na kimataifa.
Ameeleza kuwa serikali imepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, ikiwemo kuzindua Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), unaolenga kuhakikisha mtoto wa darasa la tatu anaweza kusoma, kuandika na kuhesabu kwa ufasaha.
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu ameitaka jamii kushirikiana na serikali katika kuboresha mazingira ya elimu ili kuzalisha rasilimali watu yenye ushindani.
Wakati huo huo, Dk. Nchemba ameipongeza Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Tanzania, Taifa Stars, kwa kufikia hatua ya 16 bora katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zilizofanyika nchini Morocco.
Aidha amesema mafanikio hayo yameitambulisha Tanzania kimataifa na kuongeza ari ya michezo nchini, huku akiwataka wadau kuendelea kuiunga mkono timu hiyo ya taifa.
Hata hivyo amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika sekta za kijamii, uchumi na michezo kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.
Ili kupata undani wa taarifa nyingine nyingi zaidi tufuatilie na usikilize jembe Habari Kamili ifikapo saa moja kamili jioni ambapo msomaji wetu wa hii leo ni @bfortyfive tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.
Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime