Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kesho Februari 7 mwaka huu kwa ziara ya kikazi ya siku moja yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Katika ziara hiyo, Rais Museveni atafanya mazungumzo ya ana kwa ana na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo mazungumzo yao yatajikita katika kukuza ushirikiano wa kanda, diplomasia ya kiuchumi pamoja na masuala muhimu ya kikanda na kimataifa.
Aidha miongoni mwa ajenda kuu zitakazojadiliwa ni masuala ya nishati, hususan utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unaotarajiwa kuimarisha uchumi wa Tanzania, Uganda na kanda kwa ujumla.
Hata hivyo viongozi hao pia watajadili fursa za biashara, uwekezaji, usalama wa kikanda pamoja na kuimarisha mahusiano ya muda mrefu kati ya mataifa hayo jirani.
Hivyo basi baada ya mazungumzo yao, Rais Samia na Rais Museveni wanatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari kueleza matokeo ya kikao hicho na mwelekeo wa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime