TAASISI ya Madereva wa Magari ya Abiria na Mizigo (TIMD) mkoani Mwanza imesema imepokea na kuanza kutekeleza agizo la Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, la kusimamia kanuni na taratibu za utoaji huduma kwa abiria, hususan wanafunzi wanaotumia usafiri wa umma bila kunyanyaswa.
Akizungumza na Jembe Habari, Katibu wa TIMD Mkoa wa Mwanza, Bw. Mwaka Isabuki, amesema maagizo hayo yanahusisha kuhakikisha madereva na makondakta wanazingatia haki za abiria kwa kuwaheshimu, kuwasikiliza na kuwahudumia kwa kufuata sheria elekezi za usafirishaji.
Isabuki amesema agizo hilo limekuja kufuatia video iliyosambaa mitandaoni ya mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Mariana Eric Mirindima, mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani, akieleza changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wanapotumia mabasi ya mijini maarufu kama daladala.
Ameeleza kuwa kama wadau wa usafirishaji, TIMD inatambua kuwa wanafunzi ni abiria halali wanaopaswa kuheshimiwa na kupewa nafasi zao bila kubaguliwa wala kunyanyaswa.
“Tunatambua haki ya abiria kusikilizwa, kuheshimiwa na kuhudumiwa kwa mujibu wa sheria. Tutahakikisha wanachama wetu wanazingatia maelekezo ili kuondoa changamoto za usafiri kwa wanafunzi,” amesema Isabuki.
Ameongeza kuwa TIMD itaendelea kutoa elimu kwa madereva na makondakta kuhusu umuhimu wa kufuata kanuni za usafiri wa umma, ili kuboresha huduma na kulinda usalama pamoja na ustawi wa wanafunzi na abiria kwa ujumla.
Kwa taarifa zaidi tufuatilie na usikilize jembe Habari Kamili hapo saa saba kamili mchana ambapo msomaji wetu wa hii leo ni @georgekivumbi tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.
Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime