Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemtaka mkandarasi Humphrey Construction Limited kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo la ghorofa tano katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana kwa kufanya kazi mchana na usiku ili mradi huo uanze kutoa huduma kwa wananchi kwa haraka.
RC Mtanda amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa ajili ya mradi huo, huku mkandarasi tayari akiwa ameshapokea zaidi ya shilingi milioni 900, lakini kasi ya utekelezaji hairidhishi kutokana na idadi ndogo ya wafanyakazi na uzembe katika usimamizi wa kazi.
Kwa mujibu wa mkataba ujenzi huo ulipaswa kukamilika Januari 2026, lakini hadi sasa umefikia takribani asilimia 83 ya utekelezaji. Hivyo, RC Mtanda amemtaka mkandarasi kuhakikisha awamu ya kwanza ya mradi inakamilika ifikapo Machi 11 mwaka huu kama ilivyokubaliwa.
Ameonya kuwa kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati kutamnyima mkandarasi awamu ya pili ya ujenzi na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Vilevile RC Mtanda amemtaka Mkandarasi Mshauri ATC Production and Consulting Bureau PLC ya Arusha kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo ya mradi pamoja na kusimamia viwango vya ubora ili kuepuka kasoro za ujenzi.
Akitoa taarifa ya mradi huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyamagana, Dkt. Halima Basila, amesema jengo hilo litakapokamilika litatoa huduma za dharura, ICU, maabara, huduma za mionzi, upasuaji, kliniki za macho na meno, wodi za wazazi, wodi binafsi pamoja na ofisi za utawala.
Mradi huo wa siku 365 ulianza Novemba 2024 na hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 826 zimetumika kwa mkandarasi mshauri na mjenzi, huku gharama ya mradi mzima ikikadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 14. Serikali Kuu tayari imeshatoa zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa awamu mbili kwa ajili ya utekelezaji wake.
Sasa ili kupata undani wa taarifa hii tafadhali usikose kutufuatilie na kusikiliza jembe Habari Kamili hapo saa moja kamili alasiri kamili ambapo msomaji wetu wa hii leo ni Evance Mlyakado tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.
Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime