Mtanda Asisitiza Kasi Ujenzi wa Shule ya Amali Jijini Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda,leo Februari 12 mwaka huu ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi ya Amali iliyopo Kata ya Kishiri, Jijini Mwanza, huku akiagiza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda wa wiki tatu kama ilivyopangwa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, RC Mtanda amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu, hususan elimu ya amali, ili kuwajengea watoto ujuzi wa vitendo unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

Akisoma taarifa ya mradi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Igoma, Anthony Masanja, amesema shule hiyo imepokea kiasi cha Shilingi 330,700,000 Julai 1, 2025 kupitia Mradi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi ya Amali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 75, ambapo jumla ya Shilingi 258,600,000 tayari zimetumika. Kiasi kilichobaki ni Shilingi 72,100,000 kwa ajili ya kukamilisha kazi za mwisho ikiwemo vyumba vya madarasa, ofisi na miundombinu ya huduma.

RC Mtanda amesisitiza kuwa hakuna sababu ya kuchelewesha mradi huo kwani fedha zipo, hivyo amewaagiza wasimamizi wa mradi kuongeza kasi ili shule hiyo ianze kutoa huduma kwa wakati.

“Hatupendi kuona miradi ya Serikali inakwama. Fedha zimetolewa, sasa kazi ifanyike kwa kasi na kwa ubora ili watoto wetu waanze kunufaika,” amesema RC Mtanda.

Kwa upande mwingine, RC Mtanda ametumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa wazazi, walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igoma kwa kufanya vizuri katika Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne 2025, ambapo shule hiyo imeongoza kiwilaya katika Wilaya ya Nyamagana.

Amesema mafanikio hayo yanaonyesha ushirikiano mzuri kati ya Serikali, walimu na jamii katika kuboresha elimu mkoani Mwanza.

Ili kupata undani wa taarifa hii   tufuatilie na usikilize jembe Habari Kamili hapo saa kumi kamili jioni  ambapo msomaji wetu wa hii leo ni  @GeorgeKivumbi tafadhali usipitwe na taarifa zetu Mahiri kabisa.


Lakini pia tembelea mitandao yetu ya kijamii ya Jembefmtz.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii