Rais Samia Aelekea Ethiopia Kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi wa AU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameondoka nchini leo Alhamisi Februari 12 mwaka huu kuelekea Addis Ababa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia kushiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Februari 14 hadi 15 mwaka huu.

Katika ratiba yake, Rais Samia anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC), utakaofanyika Februari 13, 2026 chini ya uenyeji wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto, kabla ya kuhudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed Ali.

Aidha, Rais Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Russell Dlamini, Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Azali Assoumani, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, pamoja na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Sidi Ould Tah, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi.

Mazungumzo hayo yanakusudia kukuza diplomasia ya kiuchumi, kuimarisha ushirikiano wa maendeleo, pamoja na nafasi ya Tanzania katika ajenda za kikanda na kimataifa.

Tanzania pia inakamilisha muda wake wa kuhudumu katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC) baada ya kulitumikia kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2022 hadi 2026, mchango uliosaidia kuimarisha amani, utulivu na usalama barani Afrika.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii