RC Chalamila Atoa Uamuzi Kunduchi – Mjane Aagizwa Kuondoka Nyumba Isiyo Mali Yake

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, ameagiza mjane aliyekuwa akidai kudhulumiwa nyumba eneo la Kunduchi kuondoka mara moja baada ya uchunguzi wa mamlaka kubaini kuwa nyumba hiyo haina umiliki halali kwake.

Uamuzi huo umetolewa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, yakihusu mgogoro wa umiliki wa nyumba kati ya mjane huyo na wadai wengine wa mali hiyo.

Baada ya kusikiliza pande zote na kupitia nyaraka husika, Serikali imebaini kuwa mjane huyo hana vielelezo vinavyothibitisha umiliki wake wa kisheria.

Akizungumza wakati wa kusikiliza sakata hilo, RC Chalamila amesema Serikali haiwezi kuruhusu mtu kuendelea kukaa au kumiliki mali isiyo yake kisheria, akisisitiza kuwa haki lazima isimamiwe kwa kuzingatia ushahidi na taratibu za ardhi.

Ameongeza kuwa migogoro mingi ya ardhi husababishwa na watu kuingia kwenye mali bila kufuata utaratibu, hali inayosababisha chuki, hasara na kuvuruga amani ya jamii.

RC Chalamila amewaagiza viongozi wa eneo hilo pamoja na vyombo vya usalama kusimamia utekelezaji wa uamuzi huo kwa kuzingatia utu, haki na usalama wa wahusika wote.

Aidha, amewahimiza wananchi kuhakikisha wanamiliki mali kwa kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kupata hati halali, mikataba na usajili sahihi ili kuepuka migogoro ya muda mrefu.

Hata hivyo hatua hiyo inalenga kuimarisha utawala wa sheria, kulinda mali za wananchi na kuzuia migogoro ya ardhi kuendelea katika Jiji la Dar es Salaam.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii