DAWATI LA JINSIA NA WATOTO NYAMAGANA LAPOKEA UGENI KUTOKA NORWAY

Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, tarehe 10 Februari 2026 limepokea ugeni kutoka nchini Norway kwa kushirikiana na wenyeji wao, Shirika la KIVULINI, kwa lengo la kujifunza na kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo.

Ugeni huo umejumuisha wajumbe wa Kamati Tendaji kutoka mashirika ya FO Innlandet na FOKUS pamoja na Mwakilishi wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania Bi. Annette Pettersen 

Mashirika hayo ni miongoni mwa wafadhili wakuu wa miradi ya kutokomeza ukatili wa kijinsia inayotekelezwa na Shirika la KIVULINI.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kiongozi wa Ujumbe, Ole Henrik Krakenes kutoka shirika la FO, amesema wamefurahishwa na kuridhishwa na kiwango cha ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza na Shirika la KIVULINI linalojihusisha na kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto. 

Baada ya kutembelea  Dawati la Jinsia na watoto Wilaya ya Nyamagana, Ole Krakenes alisema kuwa shirika lake limejifunza mambo mengi kuhusu kazi inayofanywa na KIVULINI kwa kushirikiana na wadau wake, na kwamba kuna mambo mengi yanayofanana kati ya nchi ya Norway na Tanzania katika kushughulikia masuala ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Masuala haya yanahusisha unyanyapaa, aibu, faragha na mitazamo ya jamii. Tunaona umuhimu wa kufanya kazi kwa karibu na jamii na kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya usalama na jamii,” alisema Krakenes.

Aidha, alisifu kazi nzuri inayofanywa na Shirika la KIVULINI kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, akisema ushirikiano huo ni mwelekeo sahihi kwa ustawi wa kizazi kijacho.

“Tunaamini ni muhimu kusaidia mashirika yanayofanya kazi sahihi ili kuongeza uelewa na maarifa kuhusu athari za ukatili wa majumbani na ukatili dhidi ya wanawake na watoto,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mildrid Mikkelsen alisema kuwa wamefika nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi kuhusu ushirikiano uliopo kati ya Shirika la KIVULINI na wadau mbalimbali, ikiwemo Jeshi la Polisi, katika kuzuia na kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Nimefurahishwa sana na kile nilichojifunza leo, hususan umuhimu wa kujenga uwezo na ushirikiano unaowezesha wanawake wengi kuripoti matukio ya ukatili kwa polisi,” alisema.

Aliongeza kuwa wamevutiwa na namna Jeshi la Polisi linavyofuatilia kesi hizo kwa karibu na kuzingatia hali na mahitaji ya waathirika.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, SSP Virginia Sodoka, alisema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na wananchi pamoja na taasisi zisizo za kiserikali, ikiwemo Shirika la KIVULINI, limefanikiwa kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia kwa asilimia 23.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za pamoja zikiwemo uimarishaji wa Dawati la Jinsia na Watoto, utoaji wa elimu kwa jamii, kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa kwa wahanga, pamoja na kushirikisha viongozi wa serikali za mitaa.

“Napongeza Shirika la KIVULINI kwa kuendelea kushirikiana na Dawati la Jinsia na Watoto, kwa kuunganisha nguvu za pamoja katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia kwa weledi, huruma na kwa kuzingatia haki za wahanga,” alisema SSP Sodoka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally, aliwasilisha taarifa ya shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo katika mkoa ya Mwanza, akieleza juhudi zinazoendelea kufanywa katika kuzuia na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii