MWANAMKE mmoja katika Kaunti ya Mombasa alilia haki yake huku akidai alitiliwa tindikali kwenye kinywaji chake katika baa iliyo eneo la Shanzu.
Mwanamke huyo anayejulikana kwa jina la Bi Susan Rioba alieleza kuwa, usiku wa Januari 15 mwaka huu akiwa na rafiki yake, aliagiza kinywaji cha pombe pamoja na chupa ya maji. Hata hivyo, alipohudumiwa, kile alidhani ni maji kilibainika kuwa ni asidi baada ya kuonja.
“Mhudumu alimimina kinywaji kiasi kwenye glasi na kuongeza kile alichodai ni maji. Nilipokinywa, nilihisi ladha ya ajabu na kama moto mdomoni. Nilijaribu kumeza lakini ikashindikana, nikatema. Rafiki yangu pia alionja na akatema. Tulimwita meneja, naye alipoonja, alitema pia,” alisema Bi Rioba.
Anasema alimwomba rafiki yake amkimbize hospitalini baada ya mdomo wake kuanza kuhisi kuungua.
Kulingana naye, wafanyakazi wa baa walipotambua kilichotokea, mmoja wao aliondoka na chupa iliyotiliwa shaka.
Bi Rioba anasema alipokuwa akijaribu kutoka akiwa amebeba glasi kama ushahidi, mlinzi aliigonga, na kilichokuwemo kikamwagika kwenye paja lake na kusababisha majeraha ya kuungua.
Alikimbizwa hospitali moja ya kibinafsi Shanzu saa nane usiku, akiandamana na wafanyakazi wawili wa baa hiyo, ambao baadaye waliondoka ili aripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Bamburi.
Kwa mujibu wa ripoti ya matibabu iliyoonekana na Taifa Leo, mdomo wake ulikuwa na dalili wazi za kuungua kwa kemikali katika sehemu za ndani za mashavu, ulimi na koo.
Ripoti hiyo pia ilieleza kuwa nguo zake zilitoa harufu kali inayofanana na asidi ya haidrokloriki.
Pajani, alipatikana kuwa na uvimbe mdogo na mwasho wa ngozi, kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, Bi Rioba alimuona daktari maalumu wa masikio, pua na koo kutokana na maumivu na ugumu wa kumeza.
Baadaye aliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Bamburi chini ya OB nambari 32/13/01/2026 na kujaza fomu ya P3 katika Hospitali ya Rufaa ya Coast General.
Duru katika idara ya polisi zilithibitisha kuwa tukio hilo lililohusisha Balsons Bar and Restaurant linachunguzwa, na sasa limekabidhiwa kwa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI).
Aidha wamiliki wa baa hawakupatikana kutoa maoni kuhusu tukio hilo, huku wakili wao akisema ni suala ambalo linaendelea kuangaliwa kisheria.
Bi Rioba anasema wamiliki wa baa walijaribu kuwasiliana naye ili suala hilo litatuliwe nje ya mahakama na kumtaka atoe madai yake.
Hata hivyo mnamo Februari 2 mwaka huu alipokea barua kutoka kwa mawakili wa baa hiyo wakikana kuhusika ingawa Bi Rioba anasema sasa yuko njia panda, akihofia kuwa hakuna atakayewajibika kwa tukio ambalo karibu limgharimu maisha yake.
#10YrsJembefm #Familiamoja #AhsantekwaTime