Watu saba wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi katika maoneo tofauti katika wilaya zaNkasi na Sumbawanga mkoani Rukwa.
Akizungumza na Jembe FM leo 27, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nkandasi, Given Kisantola, amesema tukio la kwanza lililotokea Februari 26 saa 9 mchana kijiji cha Nkandasi wilayani Nkasi.
Amesema katika tukio hilo, watano waliokuwa wakifanya kibarua cha kupanda maharage shambani walikufa papo hapo huku 14 kati yao walijeruhiwa baada ya kupigwa radi wakiwa wamejikinga kwenye nyumba kidogo iliyopo shambani humo.
Amesema kuwa watu hao wakiwa wanaendelea na shughuli zao, baada ya kuona mvua imeanza kunyesha waliacha kupanda maharage na kuamua kukimbilia kwenye nyumba hiyo ili kujikinga na mvua.
Amesema, wakati watu hao wakiwa wamekaa ndani ya nyumba hiyo, ghafla radi ilipiga na kusababisha vifo hivyo na kujeruhi wengine waliokuwa wamejikinga mvua katika nyumba hiyo.
Mtendaji huyo amesema kuwa waliofariki ni wanaume watatu na wanawake wawili na majeruhi walikimbizwa katika zahanati ya jeshi Milundikwa kwa ajili ya matibabu na wengi wao wanaendelea vizuri huku wengine wakiruhusiwa kurudi nyumbani.