Iran Yakiri Maelfu Kuuawa Katika Maandamano, Takwimu Zazua Mabishano

Msemaji wa idara ya mahakama ya Iran amesema hadi sasa hakuna adhabu yoyote ya kifo iliyotolewa inayohusiana na maandamano ya hivi karibuni ya kuipinga serikali.

Afisa mmoja wa serikali ya Iran amesema mchakato wa kutoa adhabu kali kwa wahusika wa maandamano ni mgumu na wa muda mrefu akieleza kuwa unaweza kuchukua miezi kadhaa hadi miaka.

Afisa huyo pia amewatuhumu baadhi ya washiriki wa maandamano hayo kuwa ni mamluki wanaodaiwa kuwa na uhusiano na mashirika ya kijasusi ya Marekani na Israel, CIA na Mossad.

Wakati huohuo afisa mwingine wa Iran aliyeomba kufichiwa jina lake amesema kuwa mamlaka zimethibitisha kuwa watu wasiopungua 5,000 wameuawa katika maandamano ya hivi karibuni nchini humo Kulingana na afisa huyo kati ya waliopoteza maisha watu ni 500 walikuwa maafisa wa usalama.

Hata hivyo takwimu za vifo zimeendelea kutofautiana kati ya vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ya Iran ambapo siku ya Jumamosi Shirika la kutetea Haki za Binadamu la HRANA lenye makao yake Marekani liliripoti kuwa idadi ya vifo imefikia watu 3,308, huku kesi zaidi ya 4,382 zikiwa bado zinafanyiwa tathmini hivyo HRANA pia ilisema kuwa zaidi ya watu 24,000 wamekamatwa tangu kuanza kwa maandamano hayo.

Kwa upande mwingine vyombo vya habari nchini  Uingereza  viliripoti Jumapili kuwa maandamano hayo yanaweza kuwa yamesababisha vifo kati ya watu 16,500 hadi 18,000.

Aidha kwa mujibu wa vyombo hivo takwimu hizo zimekusanywa kutoka kwa wahudumu wa afya katika hospitali nane na idara sita za dharura kote nchini Iran ingawa idadi kamili ya vifo bado haiwezi kuthibitishwa rasmi.

Hata hivyo tofauti kubwa ya takwimu hizo imeendelea kuzua maswali na mjadala mpana kuhusu ukubwa halisi wa madhara yaliyosababishwa na maandamano hayo, huku jumuiya ya kimataifa ikitaka uwazi zaidi kutoka kwa mamlaka za Iran.

#10YrsJembefm  #Familiamoja #AhsantekwaTime

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii