Kihongosi aagiza Mganga Mfawidhi achukuliwe hatua
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amemtaka Mganga Mfawidhi wa Halmashauri ya Itigi kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Itigi kwa kushindwa kusimamia ipasavyo kituo hicho, hali iliyosababisha baadhi ya watumishi kuwatoza wajawazito na watoto chini ya miaka mitano fedha za matibabu kinyume cha sheria.
Aidha, Kihongosi ameagiza halmashauri hiyo kuhakikisha inafuatilia kwa karibu na kuthibitisha kuwa hakuna mjamzito wala mtoto anayetoza fedha ili kupata huduma za afya, kama inavyoelekezwa na sera na miongozo ya Serikali.
Maagizo hayo yalitolewa wakati wa mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa lengo la kukutana na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi. Katika mkutano huo, Kihongosi aliwakumbusha watumishi wa umma kuwajibika ipasavyo na kutoichonganisha Serikali na wananchi kupitia vitendo vinavyokiuka sheria na maadili ya utumishi wa umma.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora. Viongozi wanakuja na kutoa maelekezo, lakini wapo watumishi wachache wenye vichwa ngumu wanaoichonganisha Serikali na wananchi. Sisi kama chama chenye wajibu wa kuisimamia Serikali hatutakubali kuona wananchi wakionewa,” alisema Kihongosi.
Akitoa ushuhuda, mkazi wa Itigi, Gabriel Paulo, alisema katika Kituo cha Afya Itigi wajawazito hutozwa fedha, akidai alimpeleka mkewe kliniki na akaelekezwa kulipa Sh 18,000 ili apatiwe kadi ya kliniki.
Mwananchi mwingine, Mwamini Silingi, alidai kumpeleka mtoto wake kupata matibabu lakini akaombwa Sh 10,000 ili aonane na daktari. Aliongeza kuwa licha ya kulipa fedha hizo, hakupatiwa risiti wala mtoto wake kufanyiwa vipimo vilivyostahili.
Akizungumzia Sera ya Afya ya mwaka 2007, Mganga Mfawidhi wa Halmashauri ya Itigi, Emanuel Malcange, alisema wajawazito na watoto wanapaswa kupata matibabu bure, na kusisitiza kuwa watumishi wanaowatoza fedha wanakiuka sheria, taratibu na miongozo ya utoaji wa huduma za afya.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii